UTAWALA WA SHERIA: UMUHIMU NA UIMARISHAJI WAKE NCHINI - HOTUBA YA DAG
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
OFISI YA MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI
UTAWALA WA SHERIA: UMUHIMU NA UIMARISHAJI WAKE NCHINI. HOTUBA ILIYOTOLEWA NA NDG. GEORGE M. MASAJU, NAIBU MWANASHERIA MKUU WA SERIKALI, WAKATI WA MAADHIMISHO YA SIKU YA SHERIA NCHINI DAR ES SALAAM, 6 FEBRUARI, 2013
Mheshimiwa Dr. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Anne Makinda, (Mb) Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Mohamed Chande Othman, Jaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania;
Waheshimiwa Majaji wa Mahakama ya Rufani;
Mheshimiwa Jaji Mkuu Mstaafu Augustino Stephen Lawrence Ramadhani; Mheshimiwa Jaji Mkuu Mstaafu Barnabas Samatta;
Mheshimiwa Mathias Chikawe, (Mb) Waziri wa Katiba na Mambo ya Sheria; Mheshimiwa Jaji Kiongozi;
Waheshimiwa Majaji wa Mahakama Kuu;
Waheshimiwa Majaji Wastaafu;
Waheshimiwa Mabalozi;
Viongozi wa Vyama vya Siasa;
Mtendaji Mkuu wa Mahakama;
Wastahiki Viongozi wa Dini na Madhehebu mbalimbali;
Mheshimiwa Msajili Mkuu, Msajili wa Mahakama ya Rufani; na Mahakama Kuu; Waheshimiwa Mahakimu wa ngazi zote;
Rais wa Chama Cha Mawakili;
Wasomi wenzangu Mawakili;
Mabibi na Mabwana;
Leo tunaadhimisha Siku ya Sheria inayoashiria kuanza kwa Mwaka Mpya wa shughuli za Mahakama ya Tanzania. Shughuli za Mahakama zinajumuisha kusikiliza mashauri na kuamua kuhusu haki na wajibu wa wadai na wadaiwa au washtaki na washtakiwa. Maadhimisho haya yanafanyika pia mikoani na wilayani. Tunafarijika kuona ushiriki wa pamoja wa Wakuu wote wa Mihimili ya dola iliyotajwa katika masharti ya Ibara ya 4 ya Katiba ya Nchi katika kuizindua siku hii. Maudhui ya siku ya sheria Mwaka huu ni; “UTAWALA WA SHERIA: UMUHIMU WA UIMARISHAJI WAKE NCHINI.”
Mhe. Rais, Utawala wa sheria ni dhana inayoelezea namna mamlaka ya nchi pamoja na Serikali yanavyotekelezwa kihalali iwapo tu yanafanywa kwa kufuata sheria. Uhalali wa vyombo vyote vya Serikali pamoja na taasisi zake sharti uwe na mizizi kwenye sheria ikiwa na maana kwamba uendeshaji wa shughuli zote za umma unatokana na sheria zilizotungwa ambazo sharti zizingatiwe na kutekelezwa ipasavyo na wananchi wote. Ndiyo maana enzi za uhai wake Mwalimu J.K.Nyerere aliwahi kutamka kwamba;
“Serikali ni sheria. Hakuna kitu kinaitwa Serikali bila sheria; na sheria zikishatungwa lazima zifuatwe.”
Aidha, Katiba yetu ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania katika ibara yake ya 26 inaelekeza kwamba kila mtu ana wajibu wa kufuata na kutii Katiba hiyo na sheria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Na kwamba kila mtu ana haki kwa kufuata utaratibu uliowekwa na sheria kuchukua hatua za kisheria kuhakikisha hifadhi ya Katiba na Sheria za nchi. Niongeze tu hapa kwamba mtu anayezungumzwa hapa ni pamoja na Serikali ambayo kwa mujibu wa Katiba yetu hiyo katika Ibara ya 4 ndiyo yenye mamlaka ya utendaji. Kwa hiyo Serikali inalo jukumu la kuhakikisha kwamba Katiba na sheria zinazotokana na Katiba hiyo zinazingatiwa na kutekelezwa ipasavyo na kila mtu nchini.
Mhe. Rais, Dhana hii ya utawala inalenga kuzuia matumizi mabaya ya madaraka na kuweka mipaka ya mamlaka ya Serikali na taasisi zake pamoja na wananchi kuishi kwa kuzingatia sheria za nchi kwa manufaa yao kijamii kiuchumi na kisiasa. Kwa ujumla utawala wa sheria ni sharti mojawapo la kustawi kwa demokrasia, na una jukumu muhimu katika kulinda na kukuza haki za binadamu, demokrasia na utawala bora na hivyo kuchochea maendeleo ya nchi.
Baadhi ya nguzo muhimu katika utawala wa sheria ni pamoja na:
(i) Mgawanyo wa madaraka (separation of powers) kati ya Utawala (executive), Bunge na Mahakama.
Madhumuni halisi ya mgawanyo huo ni kuzuia muhimili mmoja kuhodhi madaraka yote na hivyo kuwa na nguvu zaidi kuliko mhimili mwingine.
Kila mhimili umepewa uwezo na mamlaka na maeneo ya kazi na pia kufanya kazi kwa kudhibiti mhimili mwingine kupitia dhana ya checks and balances. Katiba iko juu ya mihimili yote. Mgawanyo wa adaraka hapa Tanzania umegawanyika katika mihimili mitatu ambayo ni Bunge, Utawala/Serikali na Mahakama. Ibara ya 4 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1997, inaainisha utekelezaji wa shughuli za mamlaka ya nchi na kuzigawa katika mihimili hiyo mitatu na kusisitiza kila mhimili kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia masharti yaliyomo katika Katiba.
(ii) Uhuru wa Mahakama
Utawala wa sheria unahitaji uwepo wa mahakama huru katika utoaji haki. Hii ni kutokana na ukweli kuwa mahakama ndicho chombo chenye mamlaka na kauli ya mwisho ya utoaji wa haki nchini kulingana na masharti yaliyomo kwenye Ibara ya 107A ya Katiba. Mahakama katika kutoa uamuzi wa mashauri ya madai na jinai kwa kuzingatia sheria, mahakama zitafuata kanuni mahsusi zifuatazo kama zilivyotajwa katika Ibara ya 107A(2):
a) Kutenda haki kwa wote bila kujali hali ya mtu kijamii au kiuchumi;
b) Kutochelewesha haki bila sababu ya kimsingi;
c) Kutoa fidia ipasavyo kwa watu wanaoathirika kutokana na Makosa ya watu wengine; na kwa mujibu wa sheria mahsusi iliyotungwa na Bunge;
d) Kukuza na kuendeleza usuluhishi baina ya wanaohusika katika migogoro;
e) Kutenda haki bila kufungwa kupita kiasi na masharti ya kiufundi yanayoweza kukwamisha haki kutendeka.
Aidha, Ibara ya 107B ya Katiba inaweka sharti kwamba katika kutekeleza majukumu yake ya utoaji haki, mahakama zote ziko huru na kwamba zinalazimika kuzingatia tu masharti ya Katiba na sheria za nchi. Kwa hiyo, Mahakama ni kiungo muhimu katika kulinda na kutetea utawala wa sheria.
(iii) Usawa wa watu mbele ya sheria
Watu wote wana haki na wajibu sawa mbele ya sheria. Ubaguzi usio wa haki kwa misingi ya hadhi, dini, jinsia, uanachama kisiasa au rangi haukubaliki. Nguzo hii ya usawa wa watu mbele ya sheria imewekwa katika Ibara ya 13 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hivyo, Mahakama na watekelezaji wa sheria za nchi wanapaswa kuzingatia masharti hayo ya Katiba.
(iv) Mchakato wa haki na haki za msingi (due process and natural law)
Malengo ya mchakato wa haki ni kuhakikisha kuwa haki si tu inatendeka bali ionekane kwamba imetendeka. Mchakato huo huongeza uwezekano wa kufanya maamuzi sahihi kwa kufuata sheria. Mchakato wa haki unahusisha, pamoja na mambo mengine; haki za kitawala kuongozwa na sheria; haki ya kusikilizwa; ; haki ya kufahamu mashtaka; haki ya kufahamu ushahidi unaohusika; haki ya kuwepo wakati shauri linasikilizwa na kuhoji mashahidi wanaotoa ushahidi; haki ya kujua sababu za maamuzi ya kiutawala au kimahakama; haki ya kukata rufaa au kuomba marejeo dhidi ya uaumuzi wa kiutawala au kimahakama.
(v) Dhana ya kuchukuliwa kutokuwa na hatia (presumption of innocence)
Kila mtu anadhaniwa kuwa hana hatia hadi inapothibitika vinginevyo kupitia mchakato wa haki (due process). Hivyo, hairuhusiwi na si haki kumnyoshea kidole kwa kumhukumu mtu ambaye shauri dhidi yake linachunguza na vyombo vya kiuchunguzi au kuendelea mahakamani kama inavyosisitizwa katika Ibara ya 13 (6)(b) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Vivyo hivyo kwa mashauri ambayo hayajafikishwa mahakamani au katika vyombo vya usalama wa Raia, wananchi hawapaswi kujichukulia sheria mkononi kwa kuwaadhibu wanaowatuhumu kwa uhalifu au kuanzisha fujo na uvunjifu wa amani na sheria kwa namna yoyote ile kwa madai ya kufuatilia haki zao.
(vi) Kutoadhibiwa mara mbili (double jeopardy/res judicata)
Mtu hawezi kuhukumiwa zaidi ya mara moja kwa kutenda kosa moja. Aidha, katika shauri la madai, suala ambalo limetolewa ufumbuzi na mahakama haliwezi kufunguliwa tena mahakamani. Nia hasa ni kuhakikisha mashauri yanafikia tamati na kuepusha matumizi mabaya ya mchakato wa utoaji haki.
(vii) Uhalali (Legality)
Sheria sharti ziwe halali kwa maana ya kufuata masharti ya Katiba na ziwe zimetungwa kwa kufuata taratibu za utungwaji wa sheria zilizopo kama inavyoelezwa katika Ibara ya 64(5) ya Katiba yetu;
“…..endapo sheria nyingine yoyote ikikiuka masharti yaliyomo katika Katiba hii, Katiba ndiyo itakuwa na nguvu, na sheria hiyo nyingine, kwa kiasi inachokiuka Katiba, itakuwa batili.”
(viii) Kueleweka (certainty)
Utawala wa sheria unahitaji sheria ziwe rahisi ili zieleweke kwa wananchi walio wengi katika kuzitekeleza. Sheria ambazo hazieleweki zinaposomwa na watumiaji husababisha haki kutotendeka. Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imekuwa ikitimiza jukumu hili kwa kuandika miswada ya sheria katika lugha na mtindo unaoiwezesha ieleweke kwa urahisi. Na sasa tumerasimisha utaratibu wa kuandika sheria katika lugha mbili za Kiswahili na Kiingereza.
Mhe. Rais, Nguzo hizo za utawala wa sheria zinaonyesha nafasi muhimu ya utawala wa sheria katika jamii. Mbali na umuhimu wake katika kukuza, demokrasia, siasa, haki za msingi na kuhakikisha kuwa Serikali inaongozwa na sheria badala ya watu, utawala wa sheria una nafasi katika kukuza ustawi wa jamii na maendeleo ya uchumi. Kwa kweli ni vigumu jamii kuendelea kama jamii hiyo haizingatii utawala wa sheria.
Kwa upande mwingine, jamii ambayo ina mfumo mzuri unaoeleweka katika kutatua migogoro kama ilivyo hapa kwetu ambapo Mahakama ya Tanzania imepewa mamlaka hayo, na migogoro katatuliwa kwa kufuata misingi ya sheria pasipokuwa na rushwa, hongo au kishawishi chochote ikiwemo vitendo vya uvunjifu wa amani ni dhahiri kuwa ustawi wa uwekezaji, biashara, makampuni na wananchi utakua. Kama migogoro haiwezi kutatuliwa katika jamii kwa kufuata sheria, kuna hatari ya umoja na amani kutoweka na hivyo kudunisha maendeleo yetu. Kwa msingi huo, mchango wa utawala wa sheria katika maendeleo ya jamii kiuchumi na kisiasa ni muhimu sana, na hivyo kustahili kuheshimiwa na kuzingatiwa na kila mmoja wetu.
Aidha, wanasheria wanayo nafasi kubwa katika utekelezaji wa wa utawala wa sheria. Kupitia wao wananchi hufikisha masuala yao mahakamani kwa ajili ya kusuluhishwa au kupatiwa ufumbuzi. Kwa sababu hiyo tunalo jukumu na wajibu wa kuhakikisha kwamba matumizi ya taaluma yetu ya Uanasheria yanazingatia haja ya kudumishwa kwa matakwa ya Utawala wa Sheria ipasavyo.
Mhe. Rais, Kama nilivyotangulia kusema, uhuru wa mahakama ambao umeanishwa katika Ibara ya 107B ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ni nguzo muhimu ya utawala wa sheria. Uendeshaji wa Serikali kwa kufuata misingi ya kikatiba (constitutionalism) unakuwepo pale ambapo nchi ina mahakama ambayo ni huru na maamuzi yake hayaegemei upande wowote. Mahakama inakuwa huru pale inapoweza kutoa uamuzi wake bila shinikizo lolote la kimaslahi au ushawishi kutoka Serikalini, Bunge, watu binafsi ama taasisi yoyote kwa namna yoyote ile.
Aidha, utovu wa maadili ya taaluma kwa Majaji, Wasajili, Mahakimu, Mawakili wa Serikali na Mawakili wa Kujitegemea unaweza kudhoofisha imani ya wananchi kwa mhimili huu muhimu. Jambo hili likitokea ni hatari sana kwa ustawi wa nchi yetu. Mahakama inatakiwa kuwa kimbilio la mtu anayeonewa au kudai haki ili kupata haki yake. Ndiyo maana tunao mfumo huru wa kisheria ambao watu hudai haki zao hata kama mdaiwa ni Serikali kama ambavyo tunavyoshuhudia kesi zikifunguliwa dhidi ya Serikali.
Mhe. Rais, Mwisho napenda kutoa rai kwa wanasheria wenzangu kuendeleza mfumo wa uhuru wa taaluma ya sheria tulionao katika kutekeleza utawala wa sheria kwa kuzingatia yafuatayo;-
(i) kufanya kazi kama maafisa wa mahakama, kuwasilisha matakwa ya wateja kwa ukamilifu, uadilifu na kwa mujibu wa sheria,
(ii) kulinda haki za watu hata kama ni kundi chache (minority), ili mradi haki hizo zinatambuliwa katika msingi wa Katiba na Sheria za nchi yetu.
(iii) kuanzisha mipango ya kuitaarifu jamii kuhusu haki na wajibu wao lakini bila kuhamasisha uasi dhidi ya mamlaka halali za Nchi;
(iv) kuwezesha uelewa wa sheria kupatikana na kuwafikia wananchi katika muktadha au mtazamo sahihi wa kisheria na;-
(v) Kuelimisha wananchi watambue kwamba haki na uhuru wa binadamu ambavyo misingi yake imeorodheshwa katika Katiba yetu havitatumika na mtu mmoja kwa maana ambayo itasababisha kuingiliwa kati au kukatizwa kwa haki na uhuru wa watu wengine au maslahi ya Umma.
Mhe. Rais, Mwaka 1994 katika Mkutano kuhusu Utawala wa Sheria na Vyombo vya Kikatiba (the Rule of Law and its Constitutional Organs) uliofanyika Windhoek Namibia ambapo Mheshimiwa Ismail Mohamed aliyekuwa Jaji Mkuu wa Afrika Kusini na Namibia alisisitiza ushiriki wa kila mtu katika kuimarisha utawala wa sheria pale alipotamka;
“….to survive meaningfully, the values of the constitution and the rule of law must be emotionally internalised within the psyche of citizens. The active participation of the organs of civil society outside of the constitution in the articulation and dissemination of these values is a logistical necessity for the survival and perpetuation of the rule of law.”
Inawezekana kuwa na taifa linalofuata msingi wa utawala wa sheria iwapo kila kila mtu atashiriki na kutimiza wajibu wake ipasavyo.
Asanteni sana kwa kunisikiliza.
0 comments:
Post a Comment